NYOTA ya msanii maarufu wa sinema za Tanzania, Steven Charles Kusekwa Kanumba imezimika ghafla kufuatia kuanguka chumbani kwake na kufariki dunia katika tukio linalohusishwa na ugomvi baina yake na msanii mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na hii ndiyo ripoti kamili.
CHANZO
Tukio hilo la kusikitisha na lililoacha machozi nyuma yake, lilijiri usiku wa Aprili 7, mwaka huu maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza Kijiweni, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu aitwaye Sethi Bosco, staa huyo alikuwa chumbani kwake na Lulu, baadaye alisikia kelele za mzozo kutokea huko.
Akasema, kilichofuata baada ya mzozo huo, Lulu aliondoka ghafla, yeye akaenda chumbani na kumkuta Kanumba yuko chini, bila kujua kilichomsibu.
Kijana huyo ambaye alikiri kwamba Kanumba alikuwa amekunywa pombe usiku huo, aliendelea kusema:
“Nilipofika chumbani nilimkuta (Kanumba) amekaa chini huku ameegemea ukuta. Baada ya kumchunguza nikaona anatokwa na povu na damu kinywani.
“Niliampigia simu daktari wake na kumweleza hali hiyo, naye alifika haraka na kuanza kumfanyia uchunguzi.”
AKIMBIZWA MUHIMBILI
Sethi alisema daktari alipomchunguza alishauri akimbizwe Muhimbili. “Tulipofika alifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa, alishafariki dunia muda mrefu,” alisema kwa uchungu kijana huyo.
MASTAA WAFURIKA MUHIMBILI
Habari zaidi zinasema kuwa, katika hali isiyotegemewa, mastaa mbalimbali, wakiwemo wa sinema, wacheza mpira na wanamuziki, walianza kumiminika katika hospitali hiyo ya taifa ili kujiridhisha na habari za kifo cha Kanumba.
Wengi wakiwa bado hawaamini, walipofika na kuhakikishiwa waliangua vilio, wengine kupoteza fahamu na kupewa huduma ya kwanza.
ASKARI WACHARUKA
Saa 10 alfajiri huku mastaa wakizidi kuwasili, askari wa Muhimbili walilazimika kuwaondoa waombolezaji hao kwa madai kuwa vilio vyao vilikuwa vikivuruga utaratibu mwingine wa hospitali hiyo.
Ndipo Mwenyekiti wa Bongo Movie Club, Jacob Steven ‘JB’ alipoanza kutumia nguvu ya ziada kuwataka wasanii hao kuondoka eneo hilo na kwenda nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya maombolezo na taratibu nyingine.
Hata hivyo, mpaka saa nne asubuhi bado kulikuwa na wasanii wengine wa filamu katika hospitali ya Muhimbili wakiwa hawaamini kifo cha mwenzao.
ALIKUWA NA MIPANGO YA KWENDA MAREKANI
Kwa upande wake, mama mzazi wa marehemu akiongea tokea Bukoba alikokwenda, alisema mwanaye huyo alimpigia simu hivi karibuni na kumuomba arudi Dar ili waagane kwa vile alikuwa kwenye mipango ya kwenda Marekani.
KWA NINI LULU?
Msanii wa filamu, Lulu alidakwa na maafande wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar akidaiwa kuisadia polisi kufuatia kifo cha Kanumba.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema Lulu alikamatwa kwa sababu ni mshukiwa wa kwanza wa kifo hicho kwa vile alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu usiku wa tukio.
JE, NI KWELI WALIKUWA WAPENZI KITAMBO?
Madai yaliyotua juu ya meza ya gazeti hili yanasema kuwa, Lulu na Kanumba wamekuwa wapenzi kwa muda mrefu huku wakikutana kwa siri, hali iliyozua maswali kutoka kwa watu waliokuwepo msibani hapo.
“Jamani, kwani ni kweli Lulu alikuwa mpenzi wa Kanumba? Mbona haiwezekani? Kama ni kweli basi walikuwa na siri kubwa,” alisikika akisema mwombolezaji mmoja.
Mama mwenye nyumba wa marehemu Kanumba (jina lake halikupatikana mara moja) alisema ameshamuona Lulu mara kadhaa akiwa na Kanumba nyumbani hapo.
KILICHOMUUA CHAJULIKANA
Kwa mujibu wa daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, kinachoonekana marehemu alijigonga kichwa mahali pagumu, akapata tatizo la kuvuja damu kwa ndani (internal bleeding).
Akasema kwa mtu anayepata tatizo hilo ni rahisi kufariki dunia au akipona anaweza kupatwa na ugonjwa wa kurukwa na akili.
“Kuna uwezekano mkubwa (Kanumba) angepona angeweza kuwa na tatizo la akili,” alisema daktari huyo.
MAISHA YAKE KUELEKEA KIFO
Majirani wa marehemu walisema kuwa, saa mbili usiku wa tukio, Kanumba alitoka nje akionekana mwenye hasira, baadhi ya watu wake wa karibu walimchukua na kumrudisha ndani.
Mpaka tunakwenda mitamboni, habari zinadai marehemu Kanumba anatarajiwa kuzikwa kesho jijini Dar es Salaam.
Mungu ailaze pema peponi, roho ya marehemu Steven Kanumba. Amina.
No comments:
Post a Comment
wadau unakaribishiwa kutoa comment ilimradi ziwe za kujenga na kuelimisha pia