Friday, April 20, 2012
Aibuka Mwingine tena.........soma habari zaidi
SALMA Hamidu, mkazi wa Igogo, jijini Mwanza ameibuka na kudai amezaa na marehemu Steven Kanumba mtoto wa kike aitwaye Treasure Steven Charles Kanumba (2), Ijumaa linashuka na maneno ya kinywa chake.
Akizungumza na mwandishi wetu, Salma anayefanya kazi kwenye Ofisi ya Uwakili ya Law Consultancy jijini Mwanza, alidai alianza kufahamiana na marehemu mwaka 2006 wakati yeye akiwa kwenye Kundi la Nyakato Arts chini ya Mwalimu Joseph.
CHANZO CHA UHUSIANO
Salma akasema kuwa, uhusiano wao uliunganishwa na Mwalimu Joseph ambaye alimpa marehemu namba zake za simu wakati alipopeleka filamu za Machozi Yangu na Siri Yangu kuifanyia uhariri (editing) jijini Dar es Salaam katika studio alizokuwa akifanyia kazi marehemu.
“Marehemu alipoona picha zangu kwenye filamu hizo alivutiwa na mimi katika kuigiza, akaomba namba zangu za simu kwa Mwalimu Joseph,” alisema Salma.
Mrembo huyo aliendelea kuweka wazi kuwa, baadaye Mwalimu Joseph alirejea Mwanza na kumtaka radhi kwa kumwambia alimpa Kanumba namba zake za simu.
LAIVU KWA MARA YA KWANZA
“Mwaka 2007, Kanumba aliniita Dar, alinitumia tiketi ya ndege ya Precision Air, kwetu niliaga nakwenda kumsalimia mama mkubwa anayeishi Tabata.
“Nilipofika Dar, nilimpigia simu Kanumba kumtaarifu nimefika, akanitaka tukutane Ubungo Plaza Hotel (Blue Pearl),” alisema Salma.
Pale Ubungo Plaza, marehemu kwa mara ya kwanza alimtamkia lililo moyoni mwake kwamba ametokea kumpenda na akamuomba wawe wapenzi.
“Sikuwa na uamuzi wa haraka, lakini kutokana na ushawishi wake nilikubali, baadaye nilirudi Tabata kwa mama mkubwa.
“Usiku alinipigia simu, akaniomba kesho yake tusafiri kwenda Zanzibar, nilikubali, asubuhi niliaga kwa shangaza tukaenda Zanzibar.
“Tulifikia Bwawani Hoteli. Tulikaa kwa siku tatu na kwa mara ya kwanza nilikutana na marehemu kimwili. Tuliporudi Dar mimi nikarejea Mwanza,” alisema Salma.
KANUMBA PENZI LAKOLEA, ATUA MWANZA
“Baada ya kama miezi minne na siku kadhaa hivi, marehemu alinipigia simu akasema yuko Mwanza, anataka kuja chuoni kuniona. Alikuja akiwa ameongozana na marafiki zake wawili, Credo na Theonist Rutashoborwa.
“Walikuja hadi chuoni, mimi nilitoka tukaenda kukaa kwenye baa ya Shentemba. Ilipofika saa 2 usiku, tukahamia Isamo Hotel,” alisema Salma.
Salma aliendelea kusema kuwa, pale Isamo walipata chakula kabla ya kujitupa kitandani lakini siku hiyo muda mwingi alikuwa akijisikia vibaya, marehemu akamtaka asubuhi akapime.
“Asubuhi nilikwenda kwenye Kliniki ya Dokta Ng’walida, daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto. Vipimo vilionesha nilikuwa na ujauzito wa miezi minne.
“Nilimwonesha marehemu majibu yale, hakuonekana kukubali wala kukataa, lakini baadaye akasema kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia hadi atakaponiambia.
“Baada ya siku mbili, aliaga kurejea Dar pamoja na marafiki zake. Siku chache baadaye huku nyuma kwa bahati mbaya ujauzito ulitoka, nilikwenda kwa daktari mmoja Nyakato National ambaye alithibitisha hilo. Huo ulikuwa mwaka 2008.
UJAUZITO WA PILI
Salma alisema kuwa mawasiliano na marehemu yaliendelea. Kuna siku alimpigia simu akimtaka wakutane jijini Arusha.Alipofika alipokelewa na Kanumba mwenyewe kabla ya kwenda kupiga kambi kwa rafiki yake mmoja aliyekuwa akiishi peke yake.Akasema kukutana kwao kimwili kwa safari hii, ndiko kulimpa ujauzito na hatimaye kujifungua binti anayeitwa Treasure au Tunu.
Arusha waliondoka na ndege hadi Mwanza ambapo walifikia Ladson Hotel, ipo Bwiru na kukaa kwa siku mbili kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani kwao Igoma. Akiwa na ujauzito huo, Kanumba alimtumia nauli akimtaka wakutane mjini Morogoro.“Nikiwa na tumbo langu, aliniita Morogoro, nilisafiri kwa basi hadi kule, nilifikia kwa shangazi yangu yeye alipanga kwenye hoteli ipo jirani na Kituo cha Mabasi cha Msamvu.
KANUMBA ATOA ONYO
“Kulitokea kutokuelewana kidogo na marehemu kwa sababu ya ujauzito ule, akirejea mazungumzo yake ya awali kuwa, kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia, lakini nilimwambia sina namna ya kufanya kuhusu ujauzito ule.“Hata hivyo, marehemu alinionya nisimwambie mtu kuhusu ujauzito kuwa ni wa kwake, iwe siri yangu na yake kwa sababu hakutaka habari hiyo ifike kwenye magazeti,”alisema Salma.Akaongeza: Baada ya hapo, alinipa shilingi 150,000 nikarudi nyumbani Mwanza.“Nikiwa Mwanza alikuwa akinipigia simu akitaka kujua naendeleaje na tumbo langu na kunitaka nijiandae kwa safari ya Dar, atanitumia tiketi ya ndege. “Nilisafiri, nilipofika Dar nilimjulisha, akasema tusikae Dar, twende Zanzibar. Kule tulifikia tena Bwawani Hotel. Tulikaa kwa siku nne, kisha tukarejea Dar.
Lakini tukiwa Zanzibar kuna mtu alinipigia simu na yeye akiwepo, alikasirika sana na kuninyang’anya simu, akachukua namba kisha akampigia mtu huyo, waligombana kwenye simu. Aliipasua simu yangu, akaenda kuninunulia nyingine.“Alikuwa mtu mwenye hasira, hakutaka kusikia unazungumza na simu hasa ikiwa ni sauti ya kiume. Ugomvi huo ulisababisha aikane mimba, akasema namsingizia ni ya mwanaume aliyenipigia simu. Ilifika mahali akasema kila mtu aishi kivyake.“Hata hivyo, alikuja kuniomba msamaha huku akizidi kunionya kuwa ole wangu nitangaze nina mimba yake.” Alisema ugomvi wake na Kanumba ulitokana na ujauzito na ilifika mahali Salma alimweleza mama yake ambaye alimlaumu kwa kujiingiza kwenye uhusiano na mwanaume huyo.
MISAADA KUTOKA KWA KANUMBA
Kwa upande wa misaada, Salma alisema akiwa mjamzito, marehemu alimtumia shilingi Milioni mbili na laki mbili kwa ajili ya kununua kiwanja. Baadaye alimtumia shilingi Milioni moja za kupanga nyumba. Fedha hizo alizituma kupitia Benki ya Standard Chartered Tawi la Mwanza.
Baada ya kutuma fedha hizo, marehemu aliwahi kwenda Mwanza na kufikia kwenye Hoteli ya Ryans Bay. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba.
HAKUTAKA KUPIGA NAYE PICHA
Salma anasema: Nilimtaka tupige picha ya ukumbusho akakataa, lakini nilipojifungua alikuja na kumpiga picha mtoto kwa kutumia simu yake akisema, ‘mtoto mama yangu mtupu kwani amefanana naye sana.’ Aliongeza kuwa alipojifungua Kanumba alimtumia shilingi 500,000 za matumizi ya mtoto kupitia simu ya mama yake mzazi na Salma (hakumtaja jina). Aliendelea kusema kulijitokeza sakata wakati wa kumpa jina mtoto, Kanumba akitaka amwite jina la mama yake, huku Salma naye akitaka kumwita la mama yake, ndipo wakakubaliana mtoto aitwe Treasure au Tunu ili kumaliza mzozo wa kugombea kumwita mtoto jina la upande mmoja. “Treasure alipofikisha miezi saba alisema nimpige picha nimtumie ili amwone alivyofikia, nilifanya hivyo. Siku moja akaniambia angetunga filamu kuhusu maisha yetu ambayo alipendekeza iitwe My Gift. “Siku chache kabla ya kifo chake alinipigia simu pamoja na mtoto akisema alitaka kusafiri na asingekuwepo kwa mwezi wote wa Machi mwaka huu, alimsamilia mwanaye. Lakini cha kushangaza siku chache nikapewa taarifa za kifo chake,” alisema Salma.
KWA NINI USIRI?
Salma alisema mpaka sasa anashindwa kuelewa ni kwa nini marehemu alitaka uhusiano wao uwe wa siri. Lakini baadhi ya marafiki zake walikuwa wakifahamu uhusiano huo.
NENO LA MWISHO LA SALMA
“Kanumba kaniacha njia panda, sijui la kufanya, lakini ni vyema kama angemtambulisha mwanaye kwa ndugu zake kuliko hivi sasa ambapo mengi yatazuka kuwa pengine natafuta fedha za marehemu.
“Sijaweka wazi ili nipate chochote, bali nahisi dhambi kuficha kwa sababu huyu mtoto si damu yangu peke yangu.“Nitakuwa mbaya kwa Mungu kama nisiposema ukweli. Angekuwepo mwenyewe nisingesema kwa sababu yeye ndiye alikuwa kiongozi wa maisha ya mtoto.
“Narudia tena, nina uwezo wa kumlea na wala sihitaji mtoto achukuliwe na kwenda kuishi kwa baba, ila familia ijue kuna damu yao kwangu.“Kama hawataamini, niko tayari kufika Dar na kupima DNA ili familia ya marehemu ijiridhishe,” alisema Salma.
Hata hivyo, Salma alikiri kufanya kosa la kutowahusisha marafiki wa Kanumba kumtegulia kitendawili hicho na kudai pengine umri mdogo ulichangia. Salma alizaliwa mwaka 1987.
Alisema mtu pekee ambaye watu wanamfahamu na ndiye shahidi wa uhusiano wake na marehemu ni msanii wa maigizo, Ramadhan Malele ‘Swebe’ ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara.
Salma alisema kabla Kanumba hajafikwa na mauti, yeye aliwahi kukutana na Swebe jijini Mwanza ambapo alimsimulia hali ilivyo na akamshauri kusikiliza matakwa ya marehemu ya kutotoa siri ya kuwepo kwa mtoto huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
wadau unakaribishiwa kutoa comment ilimradi ziwe za kujenga na kuelimisha pia