Saturday, March 3, 2012

BABA KANUMBA AJIBU MAPIGO

Steven Kanumba akiwa na Baba yake mzazi Mzee Charles Kuzekwa Kanumba
TAKRIBAN wiki moja tangu mwigizaji mstari wa mbele katika sinema za Bongo, Steven Charles Kanumba kuyafungukia maisha aliyoishi kwa baba yake mzazi, Charles Kusekwa Kanumba, mzee huyo amejibu mapigo, Ijumaa Wikienda linakuwa la kwanza kunasa sauti yake.
KUMBUKUMBU ZA KUSIKITISHA
Akizungumza kwa dakika 30 kwa njia ya simu kutokea Ngokolo, Shinyanga anakoishi, mzee huyo alizirarua moja kwa moja kauli za mwanaye alizozitoa kuhusu yeye alipohojiwa na Kipindi cha Take One kinachorushwa mawinguni na Runinga ya Clouds kwa msaada wa Mtangazaji Zamaradi Mketema.
AANZA KUFUNGUKA
 mzee huyo alisema: “Yote yaliyozungumzwa na Steven (Kanumba) si ya kweli na yametokana na mama yake mzazi.
“Mama yake alinikimbia nyumbani na Steven akiwa mdogo kabisa, akaenda naye Bukoba na kumficha huko hadi alipougua, akashindwa kumtibu na kumrudisha hapa Ngokolo akiwa na miaka mitatu, akanibwagia.
“Hapa nyumbani nilikuwa nimeshapata mke mwingine (anaitwa Rehema), tulimpeleka kutibiwa mpaka akapona na kupata afya, akawa kama wengine.
“Huyu mke wangu anayesema alikuwa akimtesa, ndiye aliyemlea mpaka alipofikisha umri wa kuanza darasa la kwanza.
Akiendelea kusimulia mkasa mzima, mzee huyo alisema: “Alianza shule hapahapa, akasoma hadi alipomaliza darasa la saba na kujiandaa kwenda sekondari.
“Mama yake akaja tena kumchukua, akaenda kuishi naye kwake eneo la Kambarage. Sasa anaposema sikumpa malezi mazuri, ni yapi hayo?
“Pia Steven katika kauli zake, amesema eti mimi na mama yake (wa kambo) tulikuwa tunamchungisha mbuzi na kuosha sana vyombo, wewe mwandishi hujakaa kijijini? Kuchunga mbuzi au ng’ombe mbona ni kawaida sana?
“Kusema ukweli amenidhalilisha sana. Baada ya maneno yake yale nilimpa siku tatu aniombe radhi lakini alikataa, machozi yangu kwake yapo moyoni mwangu.”
  “Unamaanisha nini kusema akuombe radhi?”
Baba Kanumba: “Kwa hizo kauli zake alizofundishwa na mama yake.”
 “Kwa nini unasema alifundishwa na mama yake? Kwani Kanumba alikuwa haoni anachofanyiwa kipindi yupo kwako?”
Baba Kanumba: “Kuosha vyombo, kuchunga mbuzi, kupika ni kumnyanyasa mtoto? Si alikuwa akifundishwa jinsi ya kuishi kwa kujitegemea?”
  “Kwani hakukuwa na watoto wengine wa kumsaidia kufanya hizo kazi hadi akawa anafanya yeye?”
Baba Kanumba: “Yeye ni mtoto wa mwisho, ilimpasa afanye kazi hizo. Tena nashangaa, amekuwa akija huku mara kwa mara na mama yake mdogo (Rehema) wanapatana sana.”
“Mara nyingi amekuwa akija huku nyumbani, nyota yake ikishuka anakuja. Mwaka jana mwezi wa 9 alikuja, nyota yake ilikuwa imefifia, nikamtafutia kizizi ikarudi tena, si unaona amekuwa maarufu zaidi.”
Ijumaa Wikienda: “Unataka kuniambia wewe ni mganga wa kienyeji?
Baba Kanumba: “Hapana, lakini najua dawa za kumfanya mwanangu azidi kuwa maarufu.”
 KANUMBA MIKONONI MWA VYOMBO VYA HABARI
Baada ya kuzungumza na mzee huyo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Kanumba na kumpasulia jipu kuhusu alichokisema baba yake.
 Kwanza alikiri namba iliyozungumza na ya vyombo vya habari ni ya baba yake, kisha kwa huzuni kubwa, msanii huyo alianza kwa kusema: “Nimesikitishwa sana na uongo ambao amezungumza baba yangu.
“Naamini kama angeangalia kipindi asingenijibu hivi. Mimi sikwenda kwenye kipindi kumsemea. Ila nilikuwa najibu maswali niliyoulizwa. Niliulizwa historia ya maisha yangu ikoje? Ndiyo nikaweka wazi.
“Anachonilaumu yeye ni kipi? Kusema ukweli? Kama anaona nimemdhalilisha, anisamehe sana, lengo langu halikuwa kumdhalilisha. Lakini ukweli utabaki palepale.
“Ikitokea siku nikaitwa kwenye runinga nyingine na kuulizwa, nitasema yaleyale kwa sababu ndiyo ukweli wangu, mimi sipendi kusema uongo.
“Anaposema mama alinibwaga kwake nikiwa na miaka 3, ni uongo, mimi nilikwenda kwa baba nikiwa darasa la 4, mkubwa kabisa.

YALIYOSITIRIKA YASEMWA
“Mbona mama alimpeleka Ustawi wa Jamii akanikana, hajawaambia? Au anadhani sijui?
“Kingine kinachoniuma ambacho sijakisema, (baba) ana tabia ya kuniomba fedha akidai anataka kufanyia kazi fulani au anakwenda kwenye matibabu, lakini kumbe sivyo.
“Halafu mbaya zaidi nikimtumia fedha anawaambia watu pale mtaani acheni nizile fedha za mjinga. Inaniuma sana.
“Pia, mimi sijawahi kwenda kwake kutaka dawa ya kukuza jina langu, kwanza wala hajui ilikuwaje nikaingia kwenye hii sanaa. Yeye alishtukia tu naonekana kwenye runinga.
“Siwezi kutumia ushirikina ili niwe maarufu, mama kanilea kwa misingi ya dini na ugomvi wetu mkubwa alikuwa akitaka kila ninaposafiri nibebe Biblia kwenye begi.”

Kuhusu kupewa siku tatu kuomba radhi?
Kanumba: “Si kweli, tangu nilipohojiwa kwenye kile kipindi hajawahi kuniambia hivyo.”

1 comment:

  1. Mmmnh!Ugomvi wa baba na mama kiujumla hatupaswi kuuongelea na hata kama ulikuwepo si vyema kuuweka hadharani kwa mtindo marehemu alioutumia.Pia kwa maelezo yake inaonekana ni kweli kabisa alikuwa kwa mama toka akiwa mdogo mpaka miaka hiyo minne.Ningekuwa na nguvu zaidi za kulisemea hilo kama ageweza sema kitu juu ya huko aliko kuwa toka akiwa mdogo mpaka miaka hiyo minne.Kunakitu nyuma ya pazia.

    ReplyDelete

wadau unakaribishiwa kutoa comment ilimradi ziwe za kujenga na kuelimisha pia